Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madai ya mateso Sri Lanka; hofu yazidi kutanda

Madai ya mateso Sri Lanka; hofu yazidi kutanda

Nchini Sri Lanka, ripoti zinaendelea kutanda juu ya madai ya kwamba mateso ni jambo la kawaida pindi polisi wanapokuwa wanafanya uchunguzi wao kwa raia. 

Taarifa hizo ni onyo kutoka kwa wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaokutana kwenye kamati ya umoja huo dhidi ya vitendo vya mateso huko Geneva, Uswisi.

Wamesema wanatiwa hofu kubwa juu ya vitendo hivyo vinavyodaiwa kufanywa na watendaji wa serikali wakitolea mfano utekwaji unaofanywa kwa kutumia kile kinachoitwa ‘Gari jeupe’, ubakaji wa wanawake na wanaume wanaotuhumiwa kuwa na uhusiano na kikundi cha Tamil Tigers.

Wakati serikali ya Sri Lanka inadai kutokuwepo kwa kambi yoyote ya siri ya mateso, kamati ya Umoja wa Mataifa dhidi ya utesaji inasema kuwa inajutia kitendo cha nchi hiyo kushindwa kueleza bayana iwapo imechunguza madai hayo ya hivi karibuni au la.