Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 2.66 zahitajika kukwamua Sahel

Dola bilioni 2.66 zahitajika kukwamua Sahel

Umoja wa Mataifa na wadau wake umezindua ombi la dola bilioni 2.66 kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kuokoa maisha kwa wakazi wa Sahel barani Afrika.

Ombi hilo limetangazwa leo huko Dakar, Senegal ambako mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwa ukanda wa Sahel Toby Lanzer amesema fedha hizo ni kwa ajili ya watu milioni 15 walioko katika nchi Nane zilizoko ukanda huo.

Amesema mamilioni ya watu kwenye ukanda huo bado wanaishi katika mazingira magumu na hivyo uhai wao utakuwa hatarini iwapo jamii ya usaidizi ya kimataifa, serikali na wadau wengine hawatosimama kidete kuwasaidia.

Bwana Lanzer ametoa mfano kuwa familia moja kati ya tano kwenye ukanda wa Sahel inaishi kifukara akisema mwakani zaidi ya watu milioni 30 watakuwa hawana uhakika wa chakula, wakati huu ambapo kiwango cha  utapiamlo kinazidi kushamiri.

Amesema Sahel imesalia na changamoto nyingi na itaendelea kuwa moja ya maeneo ya uhitaji zaidi mwaka 2017.

Nchi za ukanda wa Sahel ni pamoja na Niger, Mali, Mauritania, Chad, Burkina Faso na Senegal.