Skip to main content

Vita dhidi ya njaa vinapungua Asia Pacific:FAO

Vita dhidi ya njaa vinapungua Asia Pacific:FAO

Vita dhidi ya njaa katika ukanda wa Asia Pacific vimepungua kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa na shirika la chakula na kilimo FAO. Ukanda huo ni maskani ya asilimia karibu 60 ya watu takribani milioni 800 wanaokabiliwa na njaa kote duniani.

Tangu mwaka 1990 ukanda mzima umefanikiwa kupunguza njaa kwa nusu. FAO inasema nchi za ukanda huo ni lazima ziongeze mara mbili juhudi endapo zinataka kufikia lengo la maendeleo endelevu la kutokuwa na njaa ifikapo mwaka 2030.

Watu milioni 490 au asilimia 12 wa ukanda huo wana lishe duni wengi wao wakiwa kutoka Asia ya Kusini.Ripoti hiyo pia inaangalia ongezeko la unene wa kupindukia au utipwatipwa na kile inachokiita “njaa iliyojificha” kutokana na ukosefu wa madini mwilini.

Ripoti pia inasema katika ukanda mzima mtoto mmoja kati ya watatu ana matatizo ya kudumaa.