Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tukomeshe ukatili dhidi ya wanawake ili tukuze uchumi: Phumzile

Tukomeshe ukatili dhidi ya wanawake ili tukuze uchumi: Phumzile

Kumaliza ukatili dhidi ya wanawake kunapaswa kwenda sambamba na dhana ya uwezeshaji kwa kundi hilo, ndiyo iliyokuwa mada kuu katika mkutano hii leo uliojumuisha shirika la Umoja wa Mataifa la wanawake UN Women na shirika la biashara na viwanda IMC mjini Mumbai, India.

Katika mkutano huo uliopewa jina ‘‘Twaungana, kuwekeza katika sayari 50 kwa 50’’sekta binafsi, maafisa wa UM, wataalamu wa jinsia na wanaharakati wameeleza namna ujuzi wa maendeleo, ujasiriamali na ubunifu unavyoweza kusaidia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.

Mkutano huo umekwenda sambamba na siku 16 za harakati dhidi ya ukatili kwa wanawake na wasichana .

Mkuu wa UN Women Phumzile Mlambo-Ngcuka ameiambia hadhira hiyo kuwa ukatili dhidi ya wanawake una uhusiano wa moja kwa moja na uwezo wao wa kushiriki katika uzalishaji wa kiuchumi unaoathiriwa kwa kipato kidogo, fursa ndogo za elimu na ajira na ushiriki katika siasa.

Amesema kwa kukomesha ukatili huo, wanawake wanaweza kuzalisha na kukuza uchumi wa jamii nzima.