Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

New York yanufaika na uwepo wa makao makuu ya UM

New York yanufaika na uwepo wa makao makuu ya UM

Uwepo wa makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani umewezesha jiji hilo kujipatia zaidi ya dola bilioni tatu na nusu kila mwaka.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti iitwayo athari za Umoja wa Mataifa ya mwaka 2016  iliyotolewa hii leo na Kamishna wa masuala ya kimataifa kwenye ofisi ya meya wa jiji la New York, Penny Abeywardena.

Akiwasilisha ripoti hiyo mbele ya wanahabari, Bi. Abeywardena amesema inaonyesha faida na gharama za kiuchumi za uwepo wa Umoja wa Mataifa ikizingatia takwimu za mwaka 2014 , akisema..

(Sauti ya Abeywardena)

"Umoja wa Mataifa huchangia dola bilioni 3.69 kwenye uchumi wa jiji la New York. Kwa makadirio, ajira 25,000 za kudumu na za vibarua zinatokana na uwepo wa jumuiya ya Umoja wa Mataifa, ambapo ni ajira za moja kwa moja au zinazotokana na uwepo wa watendaji wake.”

Hata hivyo jiji la New York linagharimika kwa kuwa mwenyeji wa Umoja wa Mataifa ambapo kila mwaka hugharimika dola milioni 54 ambazo ni za usalama na kwa watendaji wake wanaoandikisha watoto wao kwenye shule za umma.

Makao makuu ya Umoja wa Mataifa yamekuwepo New York, kwa zaidi ya miongo Sita.