Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchunguzi wa ukatili wa kingono CAR umekamilika

Uchunguzi wa ukatili wa kingono CAR umekamilika

Umoja wa Mataifa umesema leo kuwa Kitengo chake cha Ndani cha Usimamizi , OIOS kimekamilisha uchunguzi wa madai ya ubakaji yaliyotokea nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR mwaka 2014 na 2015.

Umesema watuhumiwa wa madai hayo ni walinda amani kutoka Burundi na Gabon. Uchunguzi huo uliofanyika mara baada ya tuhuma hizo kuletwa mbele ya Umoja wa Mataifa Aprili, 2016. Umechukua miezi minne kukamilishwa, na umefanyika kwa ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa na nchi mbili hizo. Akizungumza na waandishi wa habari, msemaji wa Katibu Mkuu Stephan Dujarric ameongeza..

(Sauti ya Stephan)

"Umoja wa Mataifa umepeleka ripoti ya OIOS kwa nchi wanachama, Burundi na Gabon ikiwa ni pamoja na majina ya watuhumiwa na imeomba nchi hizo kuhakikisha uwajibikaji wa makosa hayo jinai."

Amesema, kwa ujumla waathirika 139 wamehojiwa na maelezo yao kurekodiwa, wakiwemo watoto wadogo 25 ambao walinajisiwa. Amesema tuhuma hizo dhidi yao zitakapohakikishwa, maafisa hao wa jeshi, hawatakubaliwa tena kutumikia oparesheni za kulinda amani.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini CAR, MINUSCA umeimarisha hatua zake za kukabiliana na ukatili wa kingono na fursa kwa jamii kutoa taarifa za unyanyasaji unaofanywa na wafanyakazi wake.