Skip to main content

Ruzuku katika nchi zinazoendelea zadororesha sekta ya uvuvi

Ruzuku katika nchi zinazoendelea zadororesha sekta ya uvuvi

Katibu Mkuu wa kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi  amesema sekta ya uvuvi katika nchi zinazoendelea inakabiliwa na uvuvi uliokithiri wenye kunufaisha wavuvi kutoka nchi zilizoendelea na hii inasababishwa na ruzuku katika sekta hiyo.

Amesema ruzuku hizo zinazokadiriwa kufikia dola bilioni 20 kwa mwaka, zinasababisha wavuvi wadogo wadogo kushindwa kushindana na meli kubwa za wavuvi kutoka nchi zilizoendelea, na matokeo yake sio tu yanaharibu sekta hizo ndogo ndogo za wavuvi bali pia kuhamishia ukosefu wa ajira kwenye nchi zinazoendelea.

Hivyo katika ripoti ya mapitio ya biashara duniani ya 2016 yenye kulenga uvuvi itakayotolewa Jumatano, Dr. Kitui amependekeza kuanzisha mikataba ya kisheria ya biashara na amesema itakuwa bora zaidi itakaposimamiwa na shirika la kimataifa la biashara WTO.

Amesema badala ya kutoa ruzuku yenye kupunguza hifadhi ya samaki wetu, ni bora kutumia fedha hizo kusimamia vizuri sekta ya uvuvi, na kujenga ajira endelevu katika uchumi wa bahari kama vile ufugaji wa samaki na utalii wa baharini.

UNCTAD ikishirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo, FAO, na Shirika la Mazingira Duniani, UNEP, wamependekeza mpango wa kumaliza madhara ya ruzuku za uvuvi, mpango ulioungwa mkono na nchi wanachama 91 na mashirika ya kiraia mwezi Julai mwaka huu.