Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano kuhusu mifumo endelevu ya chakula lakunja jamvi Roma

Kongamano kuhusu mifumo endelevu ya chakula lakunja jamvi Roma

Kongamano la kimataifa la siku mbili kuhusu mifumo endelevu ya chakula kwa ajili ya afya na kuboresha lishe, limekunja jamvi leo mjini Roma Italia.

Kongamano hilo lililowaleta pamoja watunga sera, wabunge, wataalamu wa afya na lishe kutoka serikalini na sekta binafsi, wataalamu wa maendeleo na wadau wengine liliandaliwa na shirika la chakula na kilimo duniani, FAO na shirika la afya ulimwenguni WHO.

Katika siku hizo mbili kongamano hilo limetoa fursa ya kutahimini kwa kina jinsi gani mifumo ya chakula inaweza kubadilishwa na kutoa lishe bora kwa wote.

Akizunguza wakati wa kufunga kongamano hilo mkurugenzi mkuu wa FAo Jose Graziano da Silva amesema kuna mambo muhimu manne ya kuzingatia, mosi,

(SAUTI YA GRAZIANO)

"Tunahitaji kuchagiza haraka mabadiliko katika mifumo ya chakula na mazingira ili kuweza kukabiliana na aina zote za utapiamlo na kuchagiza lishe bora. Pili tunahitaji ahadi ya dhamira ya kisiasa katika ngazi ya kitaifa ili kufikia mabadiliko haya yanayohitajika ili lishe bora iwe ajenda ya taifa."

Akaongeza tatu

(SAUTI YA GRAZIANO)

"Ni lazima tuwajengee uwezo walaji kwa kuwapatia taarifa wanazohitaji ili kuchukua uamuzi kuhusu kuchagua lishe bora. Na nne ni kwamba mabadiliko ya tabianchi ni moja au hatari kubwa ambayo tunakabiliana nayo hivi sasa na mbinu za kukabili zinapaswa kuchochewa na lishe bora.”