Skip to main content

Ulemavu wa macho si upofu wa nafsi-Stevie

Ulemavu wa macho si upofu wa nafsi-Stevie

Mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa, Stevie Wonder amesema anapigia chepuo mkataba wa kimataifa Marrakesh unaotaka machapisho ya vitabu vyote katika nukta nundu kwa kuwa kila binadamu bila kujali hali yake ana nafasi na uwezo wa kufanya ulimwengu kuwa bora kwa wote.

Akihojiwa na Radio ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani baada ya tukio la siku ya watu wenye ulemavu duniani, Wonder ambaye ni gwiji wa muziki ulimwenguni mwenye ulemavu wa macho amesema..

(Sauti ya Stevie)

“Ingawa inachukuliwa kuwa sisi tuna ulemavu, lakini bado tunasaidia watu wenye uwezo mbali mbali wasio na ulemavu. Lakini mwisho wa siku sote popote pale tulipo tuungane kwa sababu mie kuwa na ulemavu wa macho, haina maana nina upofu wa nafsi na mtu anayeona haina maana wana uwezo wa kuona mambo ya dunia tunayohitaji kuyashughulikia.”

Amesema kama isingalikuwa sera ya Marekani kuhusu vitabu vyenye maandishi ya nukta nundu asingalikuwa na ufahamu wa kuandika mashairi ya nyimbo yanayogusa watu wengi duniani hivyo..

(Sauti ya Stevie)

“Iwapo taarifa hazipatikani na sifahamu aina fulani ya muziki inatoka wapi na kwasababu siwezi kusoma na kufahamu, hivyo si jambo la haki kwa sisi kunyimwa kupata taarifa hiyo.”