Skip to main content

Afrika Kusini rekebisheni mfumo wa kuhamisha wagonjwa wa akili

Afrika Kusini rekebisheni mfumo wa kuhamisha wagonjwa wa akili

Wataalamu huru wanne wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa serikali ya Afrika Kusini kuanzisha sera na mipango ya wazi na endelevu ya kuhamisha wagonjwa wa akili kutoka hospitali kwenda uraiani.

Wametoa wito huo kufuatia tukio la hivi karibuni ambapo watu 37 kati ya 2,300 wenye matatizo ya akili walifariki dunia wakati wanahamishwa kutoka kituo cha afya cha Esidimeni kwenda kuhudumiwa na shirika moja la kiraia.

Wamesema shirika hilo la kiraia halikuwa na uwezo na vifaa vya kutosha kuwahudumia wakati wanahitaji huduma ya hali ya juu na ya uhakika bila ukomo.

Wataalamu hao wamesema ingawa mpango wa kuwezesha watu hao kupata huduma kwenye jamii ni mzuri, bado utekelezaji wake bila mipango makini inayozingatia haki za binadamu unaweza kuleta janga kama hilo la hivi karibuni.

Idara ya afya ya jimbo la Guateng tayari imeanza kuchunguza tukio hilo, sanjari na tume ya haki za binadamu nchini Afrika Kusini, wataalamu hao wakisema kuwa uchunguzi ukamilike na hatua zitakazochukuliwa kulinda haki za waathirika zitangazwe.