Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko bunge la Colombia kwa kuridhia mkataba wa amani- UM

Heko bunge la Colombia kwa kuridhia mkataba wa amani- UM

Kufuatia bunge la Colombia kuridhia mkataba mpya wa amani kati ya serikali na kikundi cha FARC-EP, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema anatiwa moyo na hatua hiyo, akipongeza pande husika na wananchi kwa azma yao ya kuwa na amani.

Taarifa ya msemaji wake imemnukuu akieleza kuwa hatua hiyo ya wananchi wa Colombia ni chachu ulimwenguni kote na kwamba kuridhiwa kwa mkataba ni hatua ya kihistoria kwa mchakato wa amani unaomaliza miongo mitano ya mapigano.

Nao wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamepongeza na kusifu uongozi thabiti ulioonyeshwa na serikali na kikundi cha FARC-EP kufanikisha mpango huo wenye maslahi kwa wananchi wote wa Colombia.

Wakati huo huo, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein amesema kuridhiwa kwa mkataba huo wa amani uliokarabatiwa ni hatua murua na hivyo ametaka pande zote pamoja na wananchi na mashirika ya kiraia kuweka tofauti zao pembeni na kuchagiza utekelezaji wake.