Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Benki ya dunia yaidhinisha dola milioni 20 kukwamua CAR

Benki ya dunia yaidhinisha dola milioni 20 kukwamua CAR

Benki ya dunia imeadhinisha dola milioni 20 kwa ajili ya kufanikisha miradi ya maendeleo huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR kwa miaka mitano ijayo.

Hatua hiyo inafuatia kikao cha bodi tendaji ya benki hiyo, ambapo katika taarifa imeelezwa kuwa fedha hizo zitasaidia kurejesha mifumo ya msingi ya usimamizi wa fedha na uwazi wakati wa kipindi hiki cha kujikwamua baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mkurugenzi wa benki ya dunia kwa nchi za Chad, Mali, Niger, Guinea na CAR Paul Noumba UM amesema zaidi ya hapo itaimarisha usimamizi wa ulipaji mishahara na vichochezi vya ukuaji uchumi.

Hata hivyo benki ya dunia imesema pamoja na fedha hizi za sasa, usaidizi zaidi wa kiufundi na uwekezaji vitaelekezwa ili kufanikisha utoaji huduma za kijamii.