Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ireland yasaidia operesheni za WFP Msumbiji

Ireland yasaidia operesheni za WFP Msumbiji

Serikali ya Ireland imetangaza leo Ijumaa mchango wa Euro milioni 1.5 kusaidia operesheni za dharura za shirika la mpango wa chakula duniani WFP nchini Msumbiji ambako watu milioni 1.4 hawawezi kukidhi mahitaji yao ya chakula kutokana na ukame uliosababishwa na El Niño.

Mchango huo umekuja wakati WFP ikiongeza msaada wa kuokoa maisha ya watu laki saba wakati msimu wa muambo ukianza nchini humo katika miezi miwili au mitatu ijayo.

Karim Manente mkurugenzi wa WFP Msumbiji ameishukuru serikali ya Ireland na kusema fedha hizo zitasaidia sana kuimarisha misaada ya kibinadamu ikiwemo kutoa mlo mashuleni, lishe na matibabu ya utapia mlo kwa watoto, wajawazito na kina mama wanaonyonyesha, na pia kusambaza chakula kwa wanaokihitaji zaidi.