Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kumbukizi ya biashara ya utumwa yalenga wakimbizi

Kumbukizi ya biashara ya utumwa yalenga wakimbizi

Leo ni siku ya kimataifa ya kukomesha utumwa, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema mafanikio ya ajenda ya 2030 yenye kipengele cha kutokomeza utumwa mamboleo hayamo katika sheria bali yamo katika kupambana na sababu ya mizizi yake.

Amesema wakati huu ni wa kukumbuka waathirika duniani kote na kutafakari mafanikio yaliyopatikana katika kuondoa aina zote za utumwa mamboleo, kama vile kazi za kulazimishwa, aina mbaya zaidi ya ajira ya watoto, ndoa za kulazimishwa na za utumishi, kazi za kitumwa na biashara haramu ya binadamu.

Ameongeza kuwa wanaoathirika zaidi ni wanawake, watoto, watu wenye asili ya Afrika, watu wa asili na wale wenye ulemavu, ambao mara nyingi hukabiliwa na unyonyaji na unyanyasaji. Vile vile amesema ongezeko la hivi karibuni la sheria zenye kuwaadhibu wale wanaokimbia vita na hali mbaya katika nchi zao vimechochea biashara ya utumwa na ulanguzi wa binadamu.

Hivyo Ban ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na wafadhili kuchangia katika mfuko wa hiari wa Umoja wa Mataifa, pamoja na kuwekeza katika miradi ya vituo vya usaidizi, ili kurejesha haki za binadamu na heshima ya maelfu ya waathirika na familia zao.

Maadhimisho ya mwaka huu yanakwenda sanjari na maadhimisho ya miaka 90 ya mkataba wa utumwa, pamoja na miaka 60 ya mkataba wa kukomesha utumwa, biashara ya utumwa, taasisi na zoezi la utumwa.