Wigo wa kupata VVU kwa barubaru umepanuka

Wigo wa kupata VVU kwa barubaru umepanuka

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF linasema barubaru 29 huambukizwa virusi vya ukimwi, VVU kila saa moja.

Katika ripoti yake mpya iliyotolewa leo, UNICEF inasema maambukizi mapya ya VVU miongoni mwa vijana yanakadiriwa kuongezeka kutoka 250,000 mwaka 2015 hadi kufikia 400,000 ifikapo mwaka 2030.

Ripoti hiyo inapandekeza mikakati ya kuongeza kasi katika kuzuia VVU miongoni mwa vijana na kutibu wale ambao tayari wameambukizwa kama vile kuwekeza katika uvumbuzi ikiwemo wa kitaifa, kuimarisha ukusanyaji wa takwimu, kutokomeza ubaguzi na unyanyasaji wa kijinsia na elimu kwa vijana.

Wakati huo huo, kumefanyika kongamano la kimataifa jijini Durban, Afrika Kusini kuhusu Ukimwi ambalo limewaleta pamoja UNICEF, wanaharakati na vijana kutoka kutoka sehemu mbali mbali Afrika kupata maoni yao. Miongoni mwao ni balozi wa vijana wa Kimataifa kuhusu Ukimwi, Mutelelenu Kalama ambaye anasema...

(Sauti ya Kalama)

" Nilijikuta na hali hiyo nilipoingia chumba cha tiba nikitaka kupima Ukimwi, na muuguzi akafunga mlango, na kipi nimefanya miezi mitatu iliyopita hadi nipime Ukimwi. Hivyo si vitu ambavyo tunavihitaji sasa, wasiniulize ni kwanini ninahitaji vitu hivyo."

UNICEF inasema mbali na mafanikio mengi yaliyopatikana, ufadhili wa fedha kwa ajili ya kukabiliana na Ukimwi umepungua tangu mwaka 2014.