Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kipindupindu Haiti; Umoja wa Mataifa waomba radhi na kuelezea mtazamo mpya

Kipindupindu Haiti; Umoja wa Mataifa waomba radhi na kuelezea mtazamo mpya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amehutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo na kuomba radhi wananchi wa Haiti kwa vifo na machungu yaliyotokana na ugonjwa wa Kipindupindu nchini humo.

Akitoa ujumbe huo mahsusi kwa lugha ya kreole na kifaransa ambazo huzungumzwa Haiti, Ban amesema…

(Sauti ya Ban)

"“Kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, naomba niseme wazi: Tunaomba radhi wananchi wa Haiti.Hatukuchukua hatua za kutosha dhidi ya mlipuko wa Kipindupindu Haiti na jinsi ulivyoenea. Tunaomba radhi kwa dhati kwa kile tulichofanya..”

image
Utoaji wa chanjo Haiti. (Picha: Logan Abassi UN/MINUSTAH)
Ban akaenda mbali akitangaza mpango mpya ikiwemo kuongeza idadi ya watoa huduma kwa kasi, mathalani idadi ya timu hizo imeongezeka kutoka 32 mwezi Aprili hadi 88 hii leo na kwamba mpango huo...

(Sauti ya Ban)

“Mpango wetu mpya Haiti una ngazi mbili. Usaidizi unaotakiwa ni karibu dola Milioni 400 katika kipindi cha miaka miwili, kukiwa kuna ngazi ya kwanza na ya pili. Ngazi ya kwanza ni harakati za kuchukua hatua kupunguza visa vya kipindupindu Haiti na ngazi ya pili inalenga moja kwa moja wananchi wa Haiti na familia zao ambao wameathirika na Kipindupindu."

image
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakitoa huduma kwa wananchi dhidi ya Kipindupindu. (Picha: Logan Abassi UN/MINUSTAH)
Amesema kilichosalia ni ufadhili wa mpango huo akisema..

(Sauti ya Ban)

"Kwa ufupi, hatua ya Umoja wa Mataifa inahitaji hatua kutoka nchi wanachama. Bila utashi wa kisiasa na ufadhili wa kifedha, tutasalia na nia njema na maneno matamu. Maneno yana nguvu, ndio! Maneno ni muhimu, ndio! lakini maneno pekee hayawezi kuchukua nafasi ya vitendo na usaidizi wa hali na mali..”

Kipindupindu kililipuka  huko Haiti mwaka 2010 na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.