Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lishe bora ni wajibu wa serikali na si mtu binafsi- FAO

Lishe bora ni wajibu wa serikali na si mtu binafsi- FAO

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO, José Graziano da Silva amesema hakuna nchi iliyo salama dhidi ya madhara ya lishe duni ambayo husababisha utapiamlo, uzito kupita kiasi au utipwatipwa.

Akifungua kongamano la siku mbili la kimataifa kuhusu mifumo endelevu ya chakula kwa ajili ya lishe bora na afya, mjini Roma, Italia, Bwana da Silva amesema lishe duni lishe duni ina gharama kubwa kijamii, kimazingira na kiuchumi.

Amesema kwa kuzingatia kuwa mtu mmoja kati ya watatu duniani ana utapiamlo, FAO inasaidia serikali kupitia mifumo ya chakula kuanzia uzalishaji, usindikaji, uuzaji hadi ulaji, na zaidi ya yote..

(Sauti ya Graziano)

“Nchi zinatarajiwa pia kuonyesha zinafanya nini au zimepanga kufanya nini kutekeleza pendekezo la mkutano wa pili wa kimataifa kuhusu lishe na hivyo kufanikisha lengo namba mbili la maendeleo endelevu. Lishe inapaswa kuboresha maisha ya watu na nina matarajio makubwa kutokana na mkutano huu.”

Katika mkutano huo, mfalme Letsie wa III wa Lesotho ambaye ametangazwa kuwa balozi mwema wa FAO kuhusu lishe huku barani Afrika akitangazwa kuwa ni bingwa wa lishe amekaribisha  hoja ya kwamba hivi sasa suala la lishe bora limejumuishwa kwenye ajenda ya kimataifa.