Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jumuiya ya kimataifa inawajibu wa kuzuia zahma Sudan Kusini:Sooka

Jumuiya ya kimataifa inawajibu wa kuzuia zahma Sudan Kusini:Sooka

Wajumbe wa tume ya haki za binadamu ya Umoja wa mataifa Sudan Kusini , wamesema Jumuiya ya kimataifa ina wajibu wa kuzuia nchi hiyo kutumbukia katika zahma kubwa. Ikihitimisha ziara ya siku 10 timu wa wajumbe watatu imeelezea mambo yanayowatia hofu ikiwemo ongezeko la hotuba za chuki, kamatakamata ya waandishi habari na watu wa asasi za kiraia, ongezeko la mgawanyiko baiaya ya makabila 64 ya nchi hiyo na uingizaji upya wa watoto vitani.

Akizungumza na waandishi wa habari mwisho wa ziara yao Jumatano mjini Juba, Bi Yasmin Sooka mwenyekiti wa tume hiyo amesema suala la utaifa limeanza kuingia dosari nchini humo

(SAUTI YA YASMIN)

“Ukizingatia kwamba nchi hii ina makabila 64, hii inatoa mwanya wa makosa ambayo taifa hili linaweza kugawanyika. Nimesikia mara kadhaa habari ya kutaka kulipiza kisasi, na mchakato wa kuzingatia watu wa kabila moja tu na jeshi na utumishi wa umma. Sambamba na hayo kuna ukweli kwamba kulazimisha kuingiza watoto vitani kunafanywa na pande zote katika mgogoro. "

Na kwa upande wa jumuiya ya kimataifa

(SAUTI YA YASMIN-2)

“Tumesema jumuiya ya kimataifa inawajibu wa kuzuia ukatili na mauaji ya halaiki, kama unavyojua mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzia mauaji ya kimbari ametoa onyo. Tunavyoona kuna dalili nyingi na viashiria lakini haimaanini haviwezi kuepukika. Kuna hatua nyingi zinaweza kuchukuliwa sasa kuepuka zahma"