Skip to main content

Siku ya Ukimwi duniani, tuangazie usaidizi kwa barubaru- Sidibé

Siku ya Ukimwi duniani, tuangazie usaidizi kwa barubaru- Sidibé

Leo ni siku ya Ukimwi duniani ambapo Umoja wa Mataifa umeelezea mshikamano wake na watu milioni 78 kote ulimwenguni wanaoishi na virusi vya Ukimwi, na kukumbuka watu milioni 35 waliofariki dunia kutokana na Ukimwi tangu kisa cha kwanza kiripotiwe miaka 35 iliyopita.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Ukimwi, UNAIDS, Michel Sidibé amesema wakati wa kuonyesha mshikamano huo ni lazima kusongesha harakati za kudhibiti maambukizi kwa mujibu wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs.

Amesema nchi zinasonga mbele kupunguza maambukizi akitolea mfano Namibia, lakini bado vijana hususan wa kike hususan nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara wako hatarini zaidi.

(Sauti ya Sidibe)

“Asilimia 90 ya maambukizi kwa barubaru ni wasichana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 19. Kiwango cha kupima ni kidogo zaidi na wako kwenye kundi ambalo hawapati huduma kwa kuwa jamii inadai kuwa bado hawajaanza mahusiano ya ngono. Kwa kuwa hawachunguzwi na huduma pia wanakosa.”

Kwa mantiki hiyo amesema ni lazima kubadili mtazamo na sera ili kuweza kufikia kundi hilo kwa uchunguzi na tiba.