Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kero kwa watoa misaada Sudan Kusini zikome: OCHA

Kero kwa watoa misaada Sudan Kusini zikome: OCHA

Mratibu wa misaada ya kibinadamu nchini Sudan Kusini Eugene Owusu anawasiwasi mkubwa na mfululizo wa hivi karibuni wa kero, ukiritimba na vikwazo vinavyowakabili watoaji misaada ya kibinadamu nchini humo.

Amesema matukio 91 wakati wa utoaji misaada yamerokodiwa kuanzia tarehe 1-28 Novemba, baadhi yake ikiwa ni matukio 64 ya unyanyasaji dhidi ya wafanyakazi wa kibinadamu na mali, 18 yakiwa ni kuingiliwa kati kwa hatua na masuala ya kiutawala, 2 zikiwa ni wafanyakazi kufukuzwa kazi.

Amesema watoa misaada ya kibinadamu wanafanya kazi bila kuchoka kila uchao kuokoa maisha na kupunguza mateso kwa wananchi, lakini bado wanakubwa na changamoto zinazozorotesha kazi zao na suala hili ni lazima lisitishwe.

Ameishukuru serikali ya Sudan Kusini kuanzisha kamati ya usimamizi wa masuala ya kibinadamu, lakini amesema matukio ya hivi karibuni hayaleti matumaini, na kusihi kuwa ahadi zilizowekwa na serikali zigeuzwe kuwa vitendo.

Kwa mantiki hiyo, ametoa wito kwa pande zote katika mzozo kuruhusu utoaji misaada ili kuwafikia watu wanaoteseka.