Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takribani nusu ya watoto Mosul hawana huduma ya maji- UNICEF

Takribani nusu ya watoto Mosul hawana huduma ya maji- UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema takribani nusu ya watoto huko Mosul, nchini Iraq hawana huduma ya maji safi baada ya bomba kuu la maji kuharibiwa wakati wa mapigano yanayoendelea. Grace Kaneiya na taarifa kamili

(TAARIFA YA GRACE)

Mwakilishi wa UNICEF nchini Iraq, Peter Hawkins amesema bomba hilo ambalo ni moja ya mabomba makuu matatu yanayotegemewa kusafirisha maji kwa raia mashariki mwa Mosul liko kwenye eneo linaloshikiliwa na kikundi cha ISIL.

Kwa sasa watoto na familia zao wako kwenye hali mbaya wakihofia kuuawa au kujeruhiwa sanjari na kukosa huduma ya maji safi na salama.

Tayari mamlaka za Iraq zinasafirisha maji kwa kutumia malori kutoka umbali wa kilometa 35 hadi makazi ya wananchi ili kuwapatia huduma hiyo adhimu.

UNICEF imeonya kuwa iwapo huduma hiyo haitarejeshwa, raia watalazimika kutumia maji yasiyo salama na hivyo kuwa hatarini kupata magojwa kama vile kipindupindu.

Bwana Hawkins amesihi pande husika kwenye mzozo kuruhusu upelekaji wa mahita ji muhimu na ukarabati, ikisema miundombinu ya kuhudumia raia haipaswi kushambuliwa.