Bado kuna nafasi ya kuivuta Yemen kutoka ukingoni: Ould Cheikh
Tangazo la Ansar Allah na chama cha siasa cha kongresi juu ya kuundwa kwa serikali mpya huko Yemen ni kikwazo kipya wakati huu wa mchakato wa amani na kwa maslahi ya watu wa nchi hiyo nyakati hizi ngumu.
Amesema mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed katika taarifa yake ya leo akisema kuwa kitendo kama hicho hakitahamasisha amani.
Amesema hatua hiyo ni kinyume na ahadi ya hivi karibuni zilizotolewa na Ansar Allah na chama cha watu cha Kongress kwa Umoja wa Mataifa na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry huko Muscat, Oman.
Akiongezea kuwa bado kuna nafasi ya kuivuta Yemen kutoka ukingoni kwa ule mpango aliouwasilisha hivi karibuni , Bwana Cheikh ameomba wawakilishi wa Ansar Allah na chama hicho cha Kongresi kuifikiria tena na kuonyesha dhamira ya mchakato wa amani na vitendo halisi.
Amesisitiza kuwa vyama lazima vishikilie maslahi ya kitaifa na kuchukua hatua za haraka ili kumaliza mgawanyiko wa kisiasa na kushughulikia usalama wa nchi hiyo, changamoto za kibinadamu na kiuchumi.
Ametoa wito kwa pande zote kuheshimu sheria na masharti ya ukomeshaji wa uhasama, mapigano ya angani na ardhini ili kuruhusu misaada ya kibinadamu na kuanza tena mazungumzo ya kuleta amani na kukomesha uharibifu na udhalimu ulioletwa na vita akisema raia wameteseka kwa muda mrefu mno.