Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makundi ya waasi acheni vurugu CAR- Ban

Makundi ya waasi acheni vurugu CAR- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-moon amesema ana wasiwasi juu ya vurugu mpya zilizofanyika wiki iliyopita huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa wakati wa ghasia hizo makundi mawili yaliyojihami ambayo zamani yalikuwa upande wa Seleka yalipambana katika mkoa wa Bria na ambapo watu kadhaa wameuawa na zaidi ya 11,000 walikimbia makazi yao.

Wengi wa waathirika ni raia, idadi kubwa ikieleza kuwa walilengwa kwa sababu ya makabila yao.

Kufuatia hali hiyo, Ban amerejelea mkutano wa hivi majuzi huko Ubelgiji kuhusu CAR akisema ni kiashiria kuwa jumuiya ya kimataifa iko tayari kuisaidia nchi hiyo ikiwa kuna ahueni na utulivu.

Ametoa wito kwa makundi ya waasi kuacha mara moja vurugu na kujishiriki kwa dhati na juhudi zinazoendelea za kushughulikia chanzo cha mgogoro ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mpango wa kusalimisha silaha na kujumuisha wapiganaji kwenye jamii,  uliopitishwa hivi karibuni kwenye mji mkuu Bangui.

Ban amesema ana matumaini kwamba mkutano maalum wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika ya Kati, utakaofanyika kesho mjini Libreville, Gabon utazungumzia juhudi zinazofanywa na serikali ya CAR na Rais Touadéra za kuimarisha amani na kuleta utulivu.