Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufaransa kuondokana na makaa ya mawe ifikapo 2023

Ufaransa kuondokana na makaa ya mawe ifikapo 2023

Rais Francois Hollande ametangaza kuwa migodi ya makaa ya mawe nchini humo itafungwa ifikapo mwaka 2023.

Tovuti ya hatua dhidi ya tabianchi inayoungwa mkono na shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP, imemnukuu Hollande akisema kuwa hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba gharama ya kuboresha vinu vya kuzalisha makaa ya mawe ni kubwa kuliko kuanzisha vyanzo vingine salama vya nishati.

Kwa sasa robo tatu ya umeme wa Ufaransa inatokana na mchanganyiko wa nishati ya nyuklia na vyanzo vingine salama, hivyo kudhihirisha kuwa makaa ya mawe hayana tena umuhimu.

Nishati itokanayo na makaa ya mawe huzalisha hewa ya ukaa mara mbili zaidi kama nishati asili kwa kiwango sawa cha umeme unaozalishwa.

Tangazo la Rais Hollande linadhihirisha azma ya Ufaransa ya kutekeleza mkataba wa Paris ambao mustakhbali wake unaonekana mashakani kufuatia kauli zilizotolewa wakati wa uchaguzi wa Marekani.

Ufaransa imesema mkataba huo hauwezi kubadilishwa huku tayari Uingereza nayo ilitangaza wiki mbili zilizopita kuwa itaondokana na makaa ya mawe ifikapo mwaka 2025, ikiwa inafuatia nyayo za Finland, Canada, Ujerumani, Uholanzi na Austria.