Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chondechonde pande za mzozo Syria rejesheni utu- O’Brien

Chondechonde pande za mzozo Syria rejesheni utu- O’Brien

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu ina wasiwasi mkubwa juu ya hatma ya raia kutokana na hali inavyozidi kuwa tete huko Aleppo, nchini Syria.

Mkuu wa ofisi hiyo Stephen O’Brien katika taarifa yake amesema mapigano ya ardhini sambamba na makombora yanayorushwa kutoka angani kwa siku kadhaa sasa yameua raia huku wengine wakiachwa na vilema.

Amesema pande kwenye mzozo wa Syria zimeonyesha kwa mara nyingine tena kuwa ziko tayari kuchukua hatua zozote ili kupata manufaa ya kijeshi kwa gharama yoyote ile hata ya uhai wa raia.

Bwana O’Brien ametoa wito kwa pande zote kwenye mzozo kurejesha utu na kuondoa vikwazo vilivyozingira maeneo na kukwamisha huduma za kibinadamu kufikia raia.

Amekumbusha kuwa hatua zozote za kuhamisha raia lazima zifanyike kwa usalama na bila kulazimishwa na kwa kuzingatia haki za binadamu na sheria za kiutu za kimataifa.