Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshikamano na wapalestina uendelee- Ban

Mshikamano na wapalestina uendelee- Ban

Leo ni siku ya kimataifa ya kuonyesha mshikamano na watu wa Palestina ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema mzozo kati ya Palestina na Israeli, si tu ni mzozo kama ilivyo mingine kwenye ukanda wa Mashariki ya Kati, bali ni mzozo uliodumu muda mrefu na kuleta makovu na mvutano kwenye eneo hilo.

Katika ujumbe wake amesema ingawa viongozi wa pande mbili hizo bado wanapazia sauti suluhu ya mataifa mawili, bado yahitajika hatua za dharura za kurejesha mchakato wa kusaka suluhu kisiasa, kuna hatari ya kwamba uwepo wa mataifa utasalia ndoto.

Ban amesema miaka ya karibuni imeshuhudia majaribio mawili bila mafanikio ya kusuluhisha mzozo huo kwa amani.

Amesema hali hiyo imeleta chuki na kukata tamaa kwa wapalestina sanjari na miongoni mwa waisraeli na hivyo ni vyema kuzingatia hatua zinazotakiwa kuweka mazingira bora ya mashauriano kwa mujibu wa ripoti ya pande nne kuhusu Mashariki ya Kati.

Kwa mantiki hiyo, Katibu Mkuu amesema katika siku hii ya kuonyesha mshikamano na wapalestina kila mtu aazimie kusongesha haki na kujenga mustakhbali wa amani, haki, usalama na utu kwa wapalestina, halikadhalika kwa waisraeli.