Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufadhili endelevu muhimu kutokomeza ukatili kwa wanawake na wasichana

Ufadhili endelevu muhimu kutokomeza ukatili kwa wanawake na wasichana

Uwekezaji katika usawa wa kijinsia, na hasa ukatili dhidi ya wanawake bado ni duni katika ukanda wa Asia Pasifiki.

Hayo yamesemwa na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana kwenye ukanda Asia-Pasifiki, maadhimisho yaliyofanyika leo huko Bangkok, Thailand.

Katibu Mtendaji wa tume ya Umoja wa Mataifa ukanda huo, ESCAP Dkt. Shamshad Akhtar amesema ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu haiwezi kufanikiwa bila kukomesha unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana.

Amesema si tu ni muhimu kwa ajili ya kufikia usawa wa kijinsia, bali pia inaathiri malengo yanayohusiana na umaskini, afya, elimu, kukosekana kwa usawa, miji endelevu, amani na haki.

Naye Dkt. Miwa Kato, Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UNWomen amesema kila mwanamke na msichana anayefanyiwa ukatili huo ana haki ya kupata huduma na msaada.

Inakadiriwa kuwa ulimwenguni mwanamke mmoja kati ya watatu anakabiliwa na ukatili katika maisha yake ilhali kwenye baadhi ya nchi za ukanda wa Asia Pasifiki asilimia 70 ya wanawake wanakumbwa na ukatili wa kimwili au kijinsia kutoka kwa wapenzi wa karibu.