Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Manusura wa mafuriko DPRK wahamia makazi mapya

Manusura wa mafuriko DPRK wahamia makazi mapya

Miezi mitatu baada ya mafuriko makubwa kukumba jimbo la kaskazini la Hamgyong katika Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea DPRK, takribani familia elfu 12 zimehamia nyumba mpya zilizojengwa ilhali familia nyingine zaidi ya elfu ya 17 zimehamia makazi yaliyofanyiwa ukarabati.

Mratibu mkazi Umoja wa Mataifa nchini humo Tapan Mishra amesema hayo leo kupitia taarifa iliyotolewa mji mkuu Pyongyang baada ya ziara ya pamoja ya wajumbe wa serikali ya DPRK na mashirika ya kibinadamu katika baadhi ya maeneo hayo.

Bwana Mishra amesema ziara yao imewapatia fursa ya kukutana na walioathirika na kujadili na mamlaka za kitaifa jinsi gani mashirika ya kibinadamu yanaweza kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kukidhi mahitaji ya msingi ya watu.

Amesema ingawa usaidizi umetolewa hususan kwenye makazi, bado usaidizi mkubwa unahitajika kwa kuwa zaidi ya hekta 27,00 0 za ardhi ya kilimo zimetwama kwenye maji.

Hadi kufikia sasa, mashirika ya kibinadamu nchini DPRK yamepata dola milioni 12 milioni ikiwemo dola milioni tano kutoka mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF.