Sudan Kusini igeni mataifa yenye makabila mengi lakini yana umoja- Løj

Sudan Kusini igeni mataifa yenye makabila mengi lakini yana umoja- Løj

Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS ambaye anamaliza muda wake Ellen Margrethe Løj amesema ameguswa sana na uvumilivu wa raia wa nchi hiyo lakini kinachomsikitisha ni kwamba matarajio yao kutokana na uhuru bado hayajatimia.

Bi. Løj amesema hayo mjini Juba, hii leo katika mkutano wake na waandishi wa habari kabla ya kuondoka nchini humo wiki hii baada ya kumaliza n’gwe yake ya miaka miwili.

Amesema ilikuwa ni heshima kubwa kwa yeye kumwakilisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini akisema..

(sauti ya Bi Løj)

“Bado hatujakamilisha kazi yetu. Hatuna amani Sudan Kusini, hatuna ustawi lakini nadhani sote ni lazima tufanye kazi kutimiza hilo. Nimeguswa sana na vile nimejifunza kuhusu Sudan Kusini, naguswa na uvumilivu wa wananchi lakini matunda ya uhuru bado. Mzozo ulioanza disemba 2013 bado unaendelea kuacha wengi bila makazi, au wakimbizi nchi jirani na nina hofu kuhusu tishio la usalama popote pale walipo na zaidi hali ngumu ya uchumi wanayolazimika kukabiliana nayo.”

Amesema jukumu la amani ni la wote, akitaka viongozi kuweka ustawi wa wananchi mbele huku akisema..

“Ni jukumu lenu wananchi wa Sudan Kusini kuketi na kujenga utambulisho wenu wa kitaifa bila kujali makabila yenu. Nawasihi mjifunze kutoka nchi nyingine za Afrika zinazofanana na Sudan Kusini, zikiwa na makabila mbali mbali lakini zimeweza kuibuka na utambulisho mmoja wa kitaifa ambao ni umoja wa kitaifa. Naweza kutoa mfano wa Afrika Kusini, Ghana na nyingine nyingi. Angalieni nchi hizo, ziwe mfano kwenu, ninyi ni wamoja ninyi ni wasudani kusini.”