Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma za afya kwa waliopoteza makazi Mosul zaimarishwa- WHO

Huduma za afya kwa waliopoteza makazi Mosul zaimarishwa- WHO

Shirika la afya ulimwenguni, WHO kwa kushirikiana na wadau wake ikiwemo mamlaka za afya nchini Iraq, wameandaa mkakati kuharakisha usaidizi kwa watu waliopoteza makazi kwenye maeneo yaliyo hatarini zaidi huko Mosul.

Mwakilishi mkazi wa WHO nchini Iraq, Alfat Musani ametaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kliniki 46 za kwenye magari, timu 45 za watoa huduma za afya wanaovinjari maeneo mbali mbali sambamba na magari 26 ya wagonjwa.

Halikadhalika huduma za kusaidia zaidi ya watu 350 000 zimetengwa ikiwemo dawa za kutibu magonjwa sugu, kuhara, vifaa vya upasuaji na tiba dhidi ya hofu na kiwewe.

Bwana Musani amesema zaidi ya watu milioni Moja na Nusu huko Mosul hawana huduma za kibinadamu tangu mwezi Juni mwaka 2014, mazingira yao ya afya yamedorora wakati huu ambapo mahitaji ya kibinadamu yanatarajiwa kuongezeka kutokana na watu wengi kukimbia Mosul.