Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nusu milioni ya watoto Syria wamezingirwa bila misaada muhimu-UNICEF

Nusu milioni ya watoto Syria wamezingirwa bila misaada muhimu-UNICEF

Ikiwa vurugu inaendelea kusambaa kote nchini Syria, idadi ya watoto waliozingirwa imeongezeka mara mbili katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja.

Takriban watoto nusu milioni kwenye maeneo 16 hawana kabisa misaada endelevu ya kibinadamu na huduma za msingi.

Hii ni kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF Anthony Lake katika taarifa yake iliyotolewa leo akisema kuwa kwa mamilioni ya raia nchini Syria, maisha yamekuwa ni kama ndoto kutokuwa na mwisho - hasa kwa mamia ya maelfu ya watoto waliozingirwa.

Bwana Lake amesema watoto wanauawa na kujeruhiwa,  wana hofu ya kwenda shule au hata kucheza nje, wakiwa pia wanapata chakula kidogo, akiongeza kuwa hii siyo njia ya kuishi, wengi wakiwa wanafariki dunia.

Huko mashariki mwa Aleppo, UNICEF inakadiria kuwa watoto 100,000 wanaishi bila misaada na wamezingirwa.

Kutokana na kukosekana kwa nafasi salama, watoto wanalazimika kugeuza maeneo ya chini ya ardhi kuwa viwanja vya michezo sambamba shule na hospitali ili waweze kuendelea kujifunza na kupata huduma ya matibabu.

Ikiwa inakaribia miaka sita tangu mzozo wa Syria ulipoanza, UNICEF imetoa wito kwa pande zote zifungue njia kuruhusu na kuwezesha kwa haraka upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa maeneo yote bila masharti.