Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Ashgabat umepata mafanikio makubwa: Wu

Mkutano wa Ashgabat umepata mafanikio makubwa: Wu

Mkuu wa Idara ya uchumi na kijamii ya Umoja wa Mataifa Wu Hongbo amesema leo kuwa wawakilishi kutoka sekta mbali mbali na wajumbe katika mkutano juu ya usafiri endelevu uliofunga pazia hii leo wamekubaliana kuwa hakutakuwepo maendeleo endelevu bila usafiri endelevu na udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi.

Bwana Wu amesema hayo huko mjini Ashgabat, nchini Turkmenistan wakati wa sherehe ya kufunga mkutano huo wa Kimataifa wa kwanza kuhusu usafiri endelevu.

Amewaambia wandishi wa habari kuwa wakati wa mkutano huo wa siku mbili aliosema ulikuwa  na mafanikio makubwa, wajumbe walichukua hatua kwa hatua kujadili na kukubaliana juu ya madhumuni ya muda mfupi na mrefu kwa ajili ya tabianchi,  malengo endelevu juu ya usafiri na hatua zinazohitaji kuchukuliwa  kwa kutumia barabara, reli, angani, meli kuendeleza mazingira na uchumi wa jamii.

Amesema wamekubaliana kuwezesha njia mpya na bunifu juu ya suala la usafiri endelevu na kuweka mbele hatua za kuimarisha utaratibu uliopo na kushirikisha mipango inayohusiana na kuendeleza siku za usoni.

Naye Gyan Chandra Acharya, Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kwa  mahitaji ya nchi maskini (UN-OHRLLS), amesema japokuwa usafiri endelevu ni changamoto kwa nchi zote lakini nchi maskini, nchi zilizo kwenye mazingira magumu ikiwemo zile zisizo na bandari na visiwa vidogo zina vikwazo fulani kama vile gharama kubwa za usafiri.