Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Castro aaga dunia, Ban atuma rambirambi

Castro aaga dunia, Ban atuma rambirambi

Rais wa zamani wa Cuba, Fidel Castro amefariki dunia Ijumaa usiku kwa saa za Cuba. Alikuwa na umri wa miaka 90.

Kufuatia taarifa hizo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesikitishwa na kifo cha Castro akisema umaarufu wake huko Amerika ya Kusini na ushawishi mkubwa aliokuwa nao katika masuala ya ulimwengu tangu akiwa Waziri Mkuu, Rais, Kamanda wa jeshi la Cuba na Katibu wa kwanza wa Chama cha Kikomunisti cha Cuba vimeacha alama kubwa katika nchi yake na juu ya siasa za kimataifa.

Amesema hayati Castro atakumbukwa kwa uongozi wake wa mapinduzi ya Cuba na kwa maendeleo katika Cuba katika nyanja za elimu, kusoma na afya na maadili yake ya mapinduzi.

Ban amesema Castro alipaza sauti kwa haki za kijamii katika majadiliano ya kimataifa akitolea mfano Baraza la Umoja wa Mataifa na vikao vya kimataifa.

Amekumbuka mkutano wake na Castro wakati wa ziara ya Cuba mwezi Januari mwaka 2014, akisema alivutiwa na uelewa wake juu ya masuala mbali mbali.

Katibu Mkuu ametuma rambirambi zake kwa watu wa Cuba na familia ya Rais huyo wa zamani, pamoja na Rais wa sasa Raul Castro akisema ana matumaini kuwa Cuba itaendelea na ustawi wa haki  za binadamu. akisema Umoja wa Mataifa utaendelea kuwa pamoja na Cuba.