Mtaalam huru atoa wito kwa DPRK na NGOs kuboresha hali ya haki za binadamu

Mtaalam huru atoa wito kwa DPRK na NGOs kuboresha hali ya haki za binadamu

Mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu huko Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK, Tomás Ojea Quintana, ametoa wito kwa serikali na mashirika ya kiraia nchini humo kuweka wananchi kwenye mipango ya mbinu zao ili kuboresha hali ya haki za binadamu.

Quintana amesema hayo katika taarifa aliyoitoa leo baada ya ziara yake ya siku 10 huko Jamhuri ya Korea au Korea Kusini na Japan .

Wakati wa ziara hiyo amekutana na kuwasikiliza watu waliokimbia DPRK, akisema amepata fursa ya kuelewa baadhi ya ukiukwaji wa haki za binadamu ambao ulihamasisha uamuzi wao wa kukimbia.

Amesifu ujasiri na ufahamu wa haki zao akisema pamoja na changamoto zote ambazo wamezipata sasa wanajiandaa kwa siku zijazo.

Hii ni safari yake ya kwanza kaskazini-mashariki mwa Asia baada ya kuteuliwa na Baraza la haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa mwezi Agosti mwaka huu.

Mtaalam huyo amebainisha kuwa baadhi ya mashirika ya kiraia yanaweka kumbukumbu ya matukio na kuelekeza mwongozo wao katika uwajibikaji ilhali wengine wanashughulikia misaada ya kibinadamu na haki za binadamu.

Atatoa ripoti kamili juu ya dhamira yake kwa Baraza la Haki za Binadamu mwezi Machi 2017.