Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto za usafiri endelevu kuangaziwa Turkmenistan

Changamoto za usafiri endelevu kuangaziwa Turkmenistan

Mkutano wa kwanza kabisa kuhusu usafiri endelevu unaanza kesho huko Ashgabat nchini Turkmenistan ukileta pamoja wawakilshi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, sekta binafsi na mashirika ya kiraia.

Lengo la mkutano huo ni kuweka mwelekeo mpya kwa usafiri endelevu duniani wakati huu ambapo sekta hiyo imetajwa kusababisha uchafuzi wa hewa unaochochea mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza na wanahabari mjini Ashgabat hii leo, msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kiuchumi na kijamii Wu Hongbo amesema hakuna shaka kuwa usafiri usio endelevu unaleta changamoto, iwe kwa mazingira na kwa binadamu.

Hivyo Bwana Wu ambaye ofisi yake ndio imeandaa mkutano huo amesema..

(Sauti ya Wu)

“Usafiri endelevu kwa upande mwingine unasaidia kuweka miundombinu ambamo kwayo tunajenga mustakhbali endelevu; inafungua fursa za biashara, ajira, masoko, elimu huduma za afya na huduma nyinginezo zinazoboresha maisha ya watu. Halikadhalika usafiri endelevu unainua wanawake na watu wenye ulemavu na wengine walio kwenye shida”

Katika mkutano huo, njia zote za usafiri ikiwemo barabara, reli, ndege, boti na meli zitajadiliwa huku shaka na shuku kwa nchi zinazoendelea na zile zisizo na bandari zikipatiwa kipaumbele.