Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ni kikwazo kwa maendeleo- Ban

Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ni kikwazo kwa maendeleo- Ban

Leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kuna ongezeko la watu kutambua kuwa vitendo hivyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu, kwa afya ya umma na kikwazo kikubwa kwa maendeleo endelevu.

Katika ujumbe wake Ban amesema hata hivyo bado kuna mengi zaidi ya kufanya kugeuza ufahamu huu katika kuzuia zaidi janga hilo.

Amesema unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana unasababisha gharama kubwa kwa familia, jamii na uchumi kwa kuwa wanawake wanashindwa kufanya kazi kutokana na vurugu, ajira zao zimo hatarini, mapato yanakwama n ahata uhuru na uwezo wao.

Katibu Mkuu amesema tangu mwaka 2008, ameongoza kampeni ya UNiTE yaani “Tuungane” ili kukomesha unyanyasaji dhidi ya wanawake, kampeni ambayo amesema inataka hatua za kimataifa za kuongeza rasilimali na kusaka ufumbuzi.

Hivyo amesema serikali zionyeshe dhamira zao na kuongeza kasi ya matumizi ya kitaifa katika maeneo yote husika, ikiwa ni pamoja na msaada wa harakati za wanawake na mashirika ya kiraia.