Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu ya wakimbizi wa Nigeria huko Cameroon wahitaji msaada- UNHCR

Maelfu ya wakimbizi wa Nigeria huko Cameroon wahitaji msaada- UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema maelfu ya wakimbizi wa Nigeria waliosaka hifadhi kwenye maeneo ya ndani zaidi kaskazini mwa Cameroon wanahitaji msaada wa dharura.

UNHCR inasema watendaji wake walitembelea wakimbizi hao mwezi huu waliosaka hifadhi ugenini kutokanana mashambulizi ya Boko Haram, na kushuhudia mazingira magumu wanamoishi na wenyeji, wengine wakilala chini ya miti au ndani ya madarasa yaliyo katika hali mbaya.

Wakimbizi zaidi ya elfu 21 kwenye maeneo ya Fotokol, Makary na Magode waliweza kusajiliwa huku UNHCR ikisema zaidi ya wakimbizi elfu 21 hawako kambini.

Leo Dobbs ni msemaji wa UNHCR Geneva, Uswisi.

(Sauti ya Leo)

“Tunasihi watu watoke kwenye maeneo ya ndani ya kaskazini karibu na mpakani na waende kwenye kambi ya Minawar ambayo iko kilometa 65 kuelekea kusini na huko kuna wakimbizi Elfu 65 na watapata  huduma za msingi wanazohitaji.”