Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha mkataba wa amani Colombia

Ban akaribisha mkataba wa amani Colombia

Hatimaye mkataba mpya wa amani umetiwa saini huko Colombia kati ya serikali na kikundi cha FARC.

Hatua hiyo imekuja baada ya mkataba wa awali uliotiwa saini mwezi Septemba kupingwa na wananchi katika kura ya maoni mwezi uliopita na hatimaye kukarabatiwa na kukamilisha shughuli ya leo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha hatua hiyo iliyotokana na mashauriano mapana na pande zote za kisiasa na kijamii nchini Colombia.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Ban amepongeza serikali ya Colombia, kikundi cha FARC-EP na wadau wote kwa hitimisho la mzozo huo wa muda mrefu.

Ban amesema anaamini hivi sasa mwelekeo ni utekelezaji akisema ghasia za hivi karibuni kwenye maeneo yaliyokuwa yameathiriwa na mzozo huo, zinawekea msisitizo ahadi zilizomo ndani ya makubaliano hayo.

Amesema ni matumaini yake kuwa wananchi wa Colombia watakuja pamoja kusongesha mbele mchakato wa amani na kwamba Umoja wa Mataifa utatoa usaidizi wote unaohitajika kupitia ujumbe wake Colombia na mashirika yake.

Wakati huo huo Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Filipo Grandi amekaribisha akisema ni matumaini makubwa kwa watu zaidi ya Milioni Saba waliokimbia makwao Colombia sasa wanaweza kurejea nyumbani.

Amesema ana matumaini kuwa hatua ya leo itafungua ukurasa mpya wa Colombia akipigie chepuo kipengele cha mkataba huo kinacholenga kuhakikisha usalama kwa viongozi wa mashirika ya kijamii na watetezi wa haki za binadamu.