Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urasimu wa vibali kwa miradi Gaza ni taabu- OCHA

Urasimu wa vibali kwa miradi Gaza ni taabu- OCHA

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Stephen O’Brien amesema operesheni za kusambaza misaada ya kibinadamu kwenye maeneo ya Palestina yanayoshikiliwa na Israeli zinazidi kukumbwa na vikwazo kila uchao.

Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana hii leo kujadili Mashariki ya Kati, hususan hoja ya Palestina, Bwana O’Brien amesema vizuizi vya Israel dhidi ya baadhi ya bidhaa zinazoonekana kuwa na matumizi zaidi ya kijeshi na pia kiraia vinakwamisha kazi yao.

Mathalani ametaja saruji, mbao na hata pampu za maji na vifaa vya mawasiliano akisema kila siku kiwango cha bidhaa zinazozuiliwa kinaongezeka.

Amesema saruji inahitajika kujenga makazi ya watu yaliyobomolewa ukanda wa Gaza wakati wa mashambulizi ya Israel na zaidi ya hapo..

(Sauti ya O’Brien)

“Siyo tu zege, miradi ya dharura yenye lengo la kupunguza madhara ya mafuriko yanayotishia watu 500,000 wakati huu majira ya baridi kali yakikaribia, nayo bado imezuiliwa kwa miezi 10 ikisubiri kibali. Miradi ya kukarabati visima vya maji na ujenzi wa kituo cha wagonjwa taabani watoto na mifano mingi ya mahitaji ya dharura ni baadhi ya vitu vilivyokumbwa na kusubiri kwa muda mrefu kusiko na lazima.”

Mkuu huyo wa OCHA amesema maendeleo ya dhati ukanda wa Gaza yanategemea kuondolewa kabisa kwa vikwazo vya Israel kwa mujibu wa maazimio ya Baraza la Usalama na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Kwa mantiki hiyo amesihi Baraza la Usalama lipigie chepuo hatua za kuhakikisha usaidizi unafikishwa ukanda wa Gaza bila vikwazo vyovyote.