Wanasiasa kuweni wakweli kuhusu biashara- Kituyi
Katibu Mkuu wa kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi amesema biashara ya kimataifa ndio njia bora zaidi kwa nchi zinazoendelea kuweka fursa za biashara na kukabili ukosefu wa usawa.
Dkt. Kituyi amesema hayo kwenye chapisho la leo la gazeti la The Guardian, wakati huu ambapo makubaliano ya biashara yaliibua hoja kwenye kampeni za uchaguzi nchini Marekani na hata kuibuka tishio la kujiondoa kwenye mkataba wa biashara wa nchi za pasifiki, TPP.
Amesema wakati wanasiasa katika nchi tajiri wanaweza kuwa na hofu juu ya biashara ya kimataifa, nchi zinazoendelea hazina mbadala zaidi ya kuimarisha uhusiano wao wa kibiashara.
Mkuu huyo wa UNCTAD ametaka wanasiasa kuwa wakweli wanapojadili gharama na faida a biashara akisema mara nyingi wanasiasa katika nchi zinazoendelea wanapokuwa wanasaka kura wanabeza biashara na hatimaye matatizo kuibuka baadaye.
Amesema biashara isiwe kisingizio cha kukosa ajira au kupungua kwa tija kwenye uzalishaji bali inaongeza fursa za ajira zinazohitajika hususan kwenye nchi zinazoendelea na ndio maana nchi hizo ikiwemo za barani Afrika zinapigia chepuo miradi jumuishi.