Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ruteere ziarani Australia kuangazia ubaguzi wa rangi

Ruteere ziarani Australia kuangazia ubaguzi wa rangi

Mtaalamu wa haki za binadamu kuhusu aina mpya za ubaguzi Mutuma Ruteere ataanza ziara nchini Australia tarehe 28 mwezi huu kufuatilia hali ya ubaguzi wa rangi nchini humo ikiwemo chuki dhidi ya wageni.

Taarifa kutoka ofisi ya haki za binadamu imemnukuu Mutuma akisema akiwa nchini humo hadi tarehe Tano mwezi ujao atazingatia zaidi hali ya ubaguzi wa watu wa jamii za asili, watu wenye asili ya bara la Afrika, wahamiaji na makundi yaliyo hatarini zaidi.

Halikadhalika atatathmini mwelekeo wa sasa wa ubaguzi, mambo yanayoibuka na pia kutathmini utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na mtaalamu wa awali Glèlè Ahanhanzo.

Ziara ya Mutuma inafuatia mwaliko wa serikali ya Australia ambapo atapata fursa ya kukagua sera za tamaduni zinazoingilia na mikakati iliyowekwa kutokomeza ubaguzi wa rangi.

Mwishoni mwa ziara hiyo itakayomkutanisha na makundi mbali mbali za kiraia na serikali, Mutuma atazungumza na wanahabari na hatimaye kuwasilisha ripoti mbele ya Baraza la Haki mwezi Juni mwakani.