Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uelewa wa hakimiliki waendelea kuongezeka duniani- WIPO

Uelewa wa hakimiliki waendelea kuongezeka duniani- WIPO

Ripoti mpya ya shirika la hakimiliki la Umoja wa Mataifa, WIPO imeonyesha kuendelea kuongezeka kwa maombi ya hataza duniani, ikiwa ni dalili ya ongezeko la uelewa wa wagunduzi kulinda haki miliki za bidhaa zao zinazoendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi.

WIPO imesema mwaka 2015 maombi Milioni 2.9 ya hataza yaliwasilishwa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.8 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

China iliibuka kidedea kwa maombi ya kwa bidhaa za ndani ilihali Marekani iliongoza kwa kusaka hataza kwa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.

Francis Gurry ni Mkurugenzi Mkuu wa WIPO amesema licha ya uchumi kudorora, kusaka hataza kumeshika kasi…

(Sauti ya Gurry)

“Kwa sababu kuna mazingira duni ya ukuaji kama tulivyoona kwa muda, lakini hapa katika WIPO tumeshuhudia ukuaji. Kwa mara nyingine tena tunaona ongezeko la maombi ya hakimiliki kutoka bara la Asia. Asilimia 62 ya maombi ya hataza duniani yametoka Asia, na takwimu kutoka China ni za aina yake na ni ofisi ya kwanza ya hataza duniani kupokea maombi Milioni Moja.”

WIPO imesema ongezeko pia limedhihirika kwenye maombi ya hakimiliki zingine kama vile nembo za biashara na ugunduzi wa bidhaa za viwandani.