Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

LGBTI wanafanyiwa ukatili na kubaguliwa: Mtaalamu UM

LGBTI wanafanyiwa ukatili na kubaguliwa: Mtaalamu UM

Watu wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, waliobadili jinsia, mashoga na wanawake wanaotembea na wanawake wenzao au LGBTI kote duniani wanaendelea kupokea lugha za chuki, ikiwa ni pamoja na kushambuliwa kwenye vyombo vya habari, kama vile vurugu na ubaguzi, amesema mtaalamu huru kuhusu ubaguzi dhidi ya LGBTI baada ya kuteuliwa na baraza la haki za binadamu.

Vitit Muntarbhorn akitoa hotuba yake ya kwanza Novemba 17 kwenye mkutano wa LGBTI ulioandaliwa na baraza la Ulaya mjini Strasbourg kama mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa amezungumzia juu ya ulinzi dhidi ya ukatili na ubaguzi kwa misingi ya mwelekeo na utambulisho wa kijinsia.

Amesema mara nyingi “watu wanataka tu kuwa wao” na bado wanakabiliana na changamoto na ukiukwaji wa haki za binadamu kote duniani. Japokuwa kuna baadhi ya mafanikio yaliyofikiwa lakini wengi bado wanakabiliwa na ukatili na ubaguzi wa kupita kiasi.

Kumekuwa na matukio ya mauaji, ubakaji, ukeketaji na ukatili mwingine ambao kumbukumbu zake ziko katika sehemu mbalimbali za dunia. Ametoa mfano kuwa mara nyingi watu hawa wanaathirika na sheria za jinai zenye mahusiano ya jinsia moja, ambazo bado zipo katika baadhi ya nchi 70, wakati mwingine wanafanyiwa ubakaji kwa nia ya kuwabadilisha hisia zao za kimapenzi.

Mtaalamu huyo ameapa kutumia mamlaka yake mapya kuhakikisha hatua zinachukuliwa chini ya kanuni ya kutobaguliwa inayotajwa katika azimio la haki za binadamu la mwaka wa 1948. Ameyataja maeneo matano muhimu ambayo yanaweza kuleta mabadiliko ambayo ni pamoja na kukubalika kwa uhusiano wa jinsia moja; utambuzi wa hadhi ya watu; kufafanua juu ya tofauti za jinsia na ngono na mafundisho ya ueleweshaji kutoka utotoni.