Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia wa Bria wakimbilia jengo la UM kusaka hifadhi

Raia wa Bria wakimbilia jengo la UM kusaka hifadhi

Raia 5000 pamoja na wafanyakazi wa serikali za mitaa na mashirika ya kibinaadamu wamekimbilia jengo la Umoja wa Mataifa katika mji wa Bria, nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, kusaka hifadhi baada ya mapigano yaliyoanza hapo jana katika mji huo.

Akizungumza na waandishi wa habari, msemaji wa Katibu Mkuu Steffan Dujarric amesema mapigano hayo yalitokea baina ya makundi ya waasi wa FPRC na UPC. Ameongeza kuwa FPRC pia lililenga jengo la Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSCA na jeshi la ujumbe huo nalo likarejesha makobora na hivyo akasisitiza..

(Sauti ya Dujarric)

“Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unasisitiza kwamba makundi haya ya waasi yatawajibishwa hususan kwa migogoro dhidi ya raia. Ujumbe huo unaonya kuhusu mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wake na majengo yake, na kwamba itakabiliana ipasavyo na vitendo vyovyote vya uhasama dhidi yake ."

MINUSCA imetoa wito kwa wadau katika mgogoro huo kusitisha mapigano haraka iwezekanavyo, na imesema imechukua hatua za kuwalinda raia na walinda amani wakati wakifanya doria.

Wadau wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wameanza kupanga utoaji msaada katika eneo hilo.