Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban amteua Luteni Generali Loitey kuwa mshauri wa kijeshi katika ulinzi wa amani

Ban amteua Luteni Generali Loitey kuwa mshauri wa kijeshi katika ulinzi wa amani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo ametangaza uteuzi wa Luteni Generali Carlos Humberto Loitey wa Uruguay kama mshauri wa kijeshi kuhusu operesheni za ulinzi wa amani.

Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu imesema mteule huyo anachukua nafasi ya Luteni Generali Maqsood Ahmed wa Pakistan. Katibu Mkuu amemshukuru Luteni Ahmed kwa juhudi zake katika kuimarisha utendaji kazi wa jeshi la Umoja wa Mataifa licha ya vikwazo kadhaa katika kazi yake ya ulinzi wa amani.

Luteni Generali Loitey ana uzoefu wa miaka zaidi ya 40 katika masuala ya kijeshi. Ameshika nafasi kadhaa ikiwamo ile ya mkuu wa ulinzi katika ubalozi wa Uruguay nchini Marekani, na amewahi kuwa Mkurgenzi Mkuu wa mfumo wa operesheni za ulinzi wa amani kitaifa nchini mwake.

Mshauri huyo kadhalika amefanya kazi katika opresheni za ulinzi wa amani kwa zaidi ya miaka mitano, hususani katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR na Chad.