Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha tamko la COP22:

Ban akaribisha tamko la COP22:

[caption id="attachment_301713" align="alignleft" width="300"]bancop22

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha tamko la mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabia nchi au COP22 uliokunja jamvi hii leo huko Marrakech, Morocco. Kwenye mkutano huo serikali nyingi zikiwakilishwa katika ngazi ya juu zimetoa tamko la Marrakech la kuchukua hatua .Tamko hilo na maamuzi mengine yaliyopitishwa yanasisitiza kuendelea kwa nguvu zote kwa juhudi za kimataifa kuunga mkono mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na kuonyesha nia kwa serikali zote utekelezaji wa mkataba huo haraka iwezekanavyo.

Kupitoa taarifa ya msemaji wake Katibu mkuu amesema nchi zote zinatambua kwamba hatua dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi ni muhimukwa usalama wao, maendeleo ya kiuchumi, kwa afya na mustakbali wa raia wao. Ameongeza kuwa hakuna nchi licha ya ukubwa au uwezo wake iliyo na kinga dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi , na hakuna nchi inayoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi peke yake.

Ban amepongeza uongozi shupavu ulioonyeshwa na baadhi ya nchi zisizojiweza nyingi zikiwa za Afrika katika kuimarisha malengo na kuchukua hatua haraka iwezekanavyo katika kuelekea asilimia 100 ya nishati safi na mustakhbali unaohimili vishindo vya tabia nchi.

Pia ametoa wito kwa nchi zilizoendelea kutimiza ahadi zao za kukusanya dola bilioni 100 kwa mwaka ifikapo mwaka 2020 ili kusaidia hatua za mabadiliko ya tabia nchi kwa nchi zinazoendelea.