Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya uvuvi duniani kuangazia utumwa kwenye sekta hiyo- FAO

Siku ya uvuvi duniani kuangazia utumwa kwenye sekta hiyo- FAO

Katika kuadhimisha siku ya uvuvi ulimwenguni tarehe 21 mwezi huu, shirika la chakula na kilimo duniani, FAO kwa kushirikiana na Holy See, wameandaa mkutano utakaofanyika roma, Italia kuangazia masuala ya utumwa baharini.

Taarifa ya FAO imesema baadhi ya mambo yatakayojadiliwa ni haja ya kuboresha mazingira ya kazi katika sekta ya uvuvi, ukiukwaji wa haki za binadamu na ajira ya watoto, maudhui yakiwa ukiukwaji wa haki za binadamu na kanuni kwenye sekta ya uvuvi.

Mkurugenzi Mkuu msaidizi wa FAO Arni Mathiesen amesema anafurahia ushirikiano wao na Vatican akisema kuwa udau wao pamoja na ule wa shirika la kazi duniani na vyama vya wavuvi unahakikisha si tu mazingira endelevu kwa uvuvi pekee bali endelevu pia kiuchumi.

Kwa mara ya kwanza kabisa, ujumbe wa kila mwaka kwa siku hiyo kwa wavuvi utatolewa moja kwa moja na Holy See kutoka makao makuu ya FAO.

Siku ya Uvuvi ulimwenguni ilianzishwa na jumuiya wavuvi mwaka 1998 kama njia mojawapo ya kusherehekea kazi hiyo inayopatia kipato watu wengi duniani.

Inakadiriwa kuwa biashara ya samaki ilileta dola bilioni 135 kwa mwaka 2015.