Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Washindi wa GEM-TECH 2016 watangazwa na ITU na UN Women

Washindi wa GEM-TECH 2016 watangazwa na ITU na UN Women

Muungano wa teknolojia ya habari na mawasiliano ITU na kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na masuala ya wanawake UN Women, leo wametoa tuzo mjini Bangkok Thailand kwa mashirika matatu.

Tuzo hiyo ya GEM-TECH 2016 imeenda kwa mashirika hayo kutokana na mchango wao mkubwa wa kujumuisha wanawake na wasichana duniani katika ulimwengu wa kidijitali na mawasiliano.

Mshindi wa kwanza ni shirika la Aliadas en Cadena kutoka Venezuela lililopokea tuzo ya matumizi ya teknolojia kwa ajili ya kuwawezesha wanawake na kuwajumuisha kidijitali. Shirika hilo limewasaidia zaidi ya wanawake 20,000 wasio na ajira kujitegemea kiuchumi kwa kuwapa mafunzo ya compyuta, mafunzo ya ajira, maendeleo binafsi, udhibiti wa fedha na kuwasaidia kuanzisha biashara.

Tuzo ya pili ya kuchagiza wanawake katika tsekta ya teknolojia imechukuliwa na shirika la utoaji elimu kwa wanawake Afrika (WAAW) kutokana na kazi zake za kutoa mafunzo ya unasihi na pia ufadhili kwa lengo la kuongeza idadi ya wanawake wanaoingia katika uongozi wa ulimwengu wa sayansi (STEM) na ubunifu wa teknolojia.

Na aliyejinyakulia tuzo ya mshindi wa tatu ya kuanzisha masuala ya utawala, sera na fursa kupitia teknolojia ni mfuko wa kimataifa uiitwao world Wide web foundation, kwa kazi zake kujitahidi kufungua mtandao wa umma kwa matumizi mazuri na kama haki ya kila mtu.

Tuzo hizo zimeandaliwa kwa ushirikiano wa jumuiya ya mtandao, Mastercard, kampuni ya Verizon, Mamlaka ya udhibiti ya Rwanda , ofisi ya mawasiliano ya Uswis, Facebook na kampuni ya VimpelCom