Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Udhibiti tabianchi wahitaji fedha zaidi- UNEP

Udhibiti tabianchi wahitaji fedha zaidi- UNEP

Umoja wa Mataifa umesema nchi tajiri zifanye kila ziwezalo kusaidia nchi maskini kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP Erik Solheim amesema hayo katika moja ya mijadala inayoendelea kwenye mkutano wa 22 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP22 huko Marrakesh, Morocco.

Amesema kwa mujibu wa mkataba wa Paris, nchi tajiri zimeahidi kuchangia dola bilioni 100 kila mwaka ifikapo mwaka 2020 kusaidia mipango ya nchi maskini kuhimili na kukabili madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo amesema ripoti ya pengo la uchangiaji ya mwaka huu wa 2016 inaonyesha kuwa gharama kwa nchi maskini kukabili madhara hayo ni kati ya dola bilioni 140 hadi bilioni 300 ifikapo mwaka 2030, au dola bilioni 280 hadi bilioni 500 ifikapo mwaka 2050, kiwango ambacho ni mara tano zaidi ya makadirio ya awali.

Mkuu huyo wa UNEP amesema kilichosalia sasa ni nchi tajiri kutimiza ahadi na kuchukua hatua zaidi za kuchangia ili pengo hilo la mahitaji lisiendelee kuongezeka.