Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali ziwe na matamanio makubwa ya kulinda tabianchi- Ban

Serikali ziwe na matamanio makubwa ya kulinda tabianchi- Ban

Kikao cha ngazi ya juu cha mkutano wa 22 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi kimefanyika hii leo huko Marrakesh, Morocco ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesihi serikali kuongeza kiwango cha mipango yao ya kitaifa ya tabianchi ifikapo mwaka 2018. Flora Nducha na ripoti kamili.

(Taarifa ya Flora)

Ban ametumia mkutano huo ambao ni wa mwisho kwake yeye, kueleza washiriki kuwa sasa si zama za kubahatisha, kwani takwimu athari kwa tabianchi zipo dhahiri, hivyo ni kujiandaa kuchukua hatua madhubuti.

Amesema sambamba na serikali, sekta binafsi nayo ichukue hatua zaidi na kianze kipindi cha mpito cha kuondokana na nishati ya kisuku huku nishati salama ikianza kutumika.

Ban alizungumza pia na wanahabari ambapo alipigia chepuo hatua zilizoanza kuchukuliwa ikiwemo ushiriki wa pande mbali mbali katika kufanikisha mkataba wa Paris…

(Sauti ya Ban)

"Miji, wananchi, watendaji wakuu wa kampuni wamekuwa chachu kubwa katiak kusaka ushawishi wa kisiasa kwenye mkataba wa Paris. Wamekuwa mstari wa mbele pia katika kusaka shughuli za kiuchumi zitoazo kiwango kidogo cha hewa ya ukaa na zinazohimili mabadiliko ya tabianchi, shughuli ambazo zitastawi kwenye dunia iliyokabiliwa na mabadiliko ya tabianchi. Sekta ya biashara inaweza kuchukua hatua zaidi kunufaika na fursa zilizopo.”

Ametolea mfano fursa za njia za usafirishaji zisizoharibu mazingira sambamba na kilimo hai.